logo

KIWANJA CHA NDEGE TABORA KUKAMILIKA MWISHO WA MWEZI -ENG. KASEKENYA

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi M/s Beijing Construction Engineering Group Co. Ltd (BCEG), anayejenga Kiwanja cha ndege cha Tabora kuhakikisha kinakamilika ifikapo Februari 28 mwaka huu.

.

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi huo Eng. Kasekenya ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi asilimia 90 hadi hivi sasa.

"Mkifanya bidii asilimia 10 zilizobaki mtakamilisha ndani ya mwezi huu na hivyo kutupa fursa ya kuwaalika viongozi wakuu kuja kufungua kiwanja hiki", amesema Eng. Kasekenya.

Naibu Waziri huyo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shillingi bilioni 24.6 kukarabati na kuboresha kiwanja hicho na kusisitiza umuhimu wa wananchi wa mkoa wa Tabora kuibua fursa za uwekezaji na biashara zitakazosababishwa na uwepo wa kiwanja cha ndege cha kisasa.

Amesema katika kurahisisha usafiri wa anga katika mikoa ya kanda ya magharibi viwanja vya ndege vya Kigoma, Sumbawanga na Shinyanga navyo vinajegwa sambamba na Tabora.

Aidha, Eng. Kasekenya amemtaka Meneja TANROADS mkoa wa Tabora kuhakikisha kukamilika kwa kiwanja hicho kunaendana na barabara bora za kwenda katika kiwanja hicho ili kuleta tija.

Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS mkoa wa Tabora Eng. Rafael Mlimaji amesema kukamilika kwa ujenzi huo unaohusisha Jengo la abiria, mnara wa kuongozea ndege, maegesho,, uzio, kituo cha hali ya hewa na barabara za kuingia kiwanjani utachochea uchumi wa mkoa wa Tabora.

"Kiwanja hiki kitarahisisha huduma za usafiri, kukuza biashara, kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kukuza utalii", amesisitiza Eng. Mlimaji.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn