MOROGORO, MAKAMBAKO, MBEYA KUTUMIKA KUSHUSHA MAFUTA KUTUMIA BOMBA LA MAFUTA -DKT.BITEKO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha kunakuwa na uendelevu wa upatikanaji wa mafuta kwa wakati wote kwa gharama halisi, kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria na kutatua malalamiko ya wateja kwa haraka ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania.
“Nawahakikishia kuwa wakati wote Serikali itaendelea kuwapa kila aina ya ushirikiano ili muweze kuwahudumia Watanzania, Serikali yoyote inapata heshima ikiwa inawahudumia wananchi ambao wana umeme na mafuta wakati wote hivyo, fanyeni kazi kwa kufuata sheria ili muwe salama, msikubali kuingiliwa na kupindisha misingi ya kazi.” alisema Dkt. Biteko
Amesema hayo Februari 17, 2025 jijini Tanga wakati akifungua Kikao cha Nne cha Baraza la Pili la EWURA.
Dkt. Biteko ameipongeza EWURA kwa kutekeleza maagizo yake aliyoyatoa wakati wa kikao cha Baraza kilichofanyika mwezi Novemba 2024 ikiwemo kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko ya wateja, kuondoa urasimu katika utoaji wa vibali vya ujenzi wa vituo vya kujazia gesi kwenye magari ( CNG), kupunguza gharama ujenzi wa vituo vya CNG, kulegeza masharti ya ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Kutokana na maagizo hayo ya Dkt. Biteko, kati ya Novemba 2024 na Januari 2025 EWURA imetoa vibali vya ujenzi wa vituo vinane vya CNG huku wawekezaji 50 wakionesha nia ya kujenga vituo vingine.
Aidha, EWURA imeshusha gharama za leseni na vibali vya ujenzi vituo vya CNG na gharama za maombi ya vibali zimepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000 na gharama za maombi ya leseni zimeshushwa kutoka 1,000,000 hadi 100,000.
Dkt. Biteko pia ametoa maagizo mbalimbali kwa uongozi wa EWURA ikiwemo kusimamia malipo na stahiki zote za kifedha za watumishi, kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa kuwa na vifaa na vitendea kazi vya kisasa vinavyoendana na muda, teknolojia na mahitaji yaliyopo kwa Taasisi na watumishi.
Maagizo mengine aliyoyatoa ni kuwaendeleza watumishi kitaaluma kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu, mfupi na wa kati katika fani mbalimbali ili kuisaidia Taasisi na watumishi kuendana na mabadiliko na maendeleo ya Teknolojia yanayotokea ulimwenguni. Pamoja na kuboresha uhusiano kati ya uongozi na watumishi kwa kuanzisha mijadala ya wazi kuhusu maendelo na mipango ya baadaye ya Taasisi.
“ Pia ni muhimu kutambua na kuthamini kazi nzuri za watumishi, vitu kama vyeti, barua za pongezi na tuzo za ufanisi husaidia kuwafanya watumishi watambue kwamba wanathaminiwa na hivyo kuendelea kuongeza bidii." Amesema Dkt. Biteko
Vilevile, amesisitiza suala la motisha kwa wafanyakazi na kuanzisha utamaduni wa kufanya mazoezi na kushiriki michezo ndani ya taasisi na kwa kushirikiana na Taasisi nyingine.
Katika kikao hicho ambacho kitajadili bajeti ijayo ya mwaka 2025/26 na utekelezaji wa bajeti ya 2024/2025, Dkt. Biteko amewahimiza wajumbe kujadili utekelezaji wa malengo ya taasisi
kwa kuzingatia ajenda ya Taifa katika masuala ya Nishati hususani matumizi ya nishati safi ya kupikia na upatikanaji wa maji kwa gharama inayostahili kwa wananchi wote.
“Naamini mtafanya tathmini kutoka katika Bajeti iliyopita na kuona ni nini tufanye ili kukidhi mahitaji ya Watanzania" alisema Biteko.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amesema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipatia nchi heshima kubwa kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kwa ajili ya kufadhili miradi hiyo.
Ameendelea “ EWURA mnatakiwa kubeba ajenda hii ya nishati safi kwa kuelimisha umma kuhusu manufaa yake, pamoja na nishati safi ya kupikia tunataka kuongeza matenki ya kushusha mafuta maeneo kama Mbeya, Morogoro na Makambako ili tuweze kuondoa changamoto ya magari yote kuja kupakia mafuta Dar es Salaam.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt.Batilda Buriani amesema kuwa EWURA imeendelea kusimamia ipasavyo mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kuhakikisha kunakuwa na ushiriki kamilifu wa wazawa na maslahi mengine ya nchi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

