Top news
MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJISAFI NALA DODOMA
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amewataka wananchi wa Kata ya Nala, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.
Ametoa wito huo wakati akiweka Jiwe la Msingi katika Mradi wa Majisafi Nala unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.4.
Pia ameitaka DUWASA kuishirikisha jamii pindi changamoto ya maji inapotokea ili kuondoa taharuki na malalamiko kwa kukosekana kwa taarifa rasmi ya sababu zinazosababisha kutokuwepo kwa maji.
"Nitoe wito kwa wananchi wa Nala, mradi huu umewekezwa fedha nyingi kwa ajili ya kuwasaidia kuondokana na adha ya maji, sasa kazi yenu ni kuhakikisha mnautunza ili uweze kudumu,"amesisitiza Ussi.
Akisoma Taarifa ya Utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema gharama ya awamu ya kwanza ya mradi ni shilingi Bilioni 1.4.
Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, amesema eneo la Nala lilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, hivyo utekelezaji wa mradi huo utasaidia sana wananchi wa eneo hilo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mkoa wa Dodoma, leo Aprili 26,2025 unakimbizwa katika Wilaya ya Dodoma Mjini na Mradi wa Majisafi Nala ni moja kati ya miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru.
Kauli Mbiu ya mwaka huu ya mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa ni "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kwa Amani na Utulivu"
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

