logo

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA MWAKA 2024/2025

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/2026 ya kiasi cha shilingi Trilioni 2.2 ambapo asilimia 96.5 ya Bajeti yote ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na asilimia 3.5 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.

Akiwasilisha Bajeti hiyo tarehe 28 Aprili, 2025 bungeni jijini Dodoma, Dkt.Biteko ametaja vipaumbele mbalimbali vya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2025/2026 ikiwemo kuendelea kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, pamoja na kufikisha Gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara.

“ Mhe. Spika, kipaumbele kingine ni kuendelea na usambazaji wa nishati katika vitongoji, maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji pamoja na vituo vya afya ili kuwezesha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.” Ameeleza Dkt.Biteko

Ametaja kipaumbele kingine kuwa ni upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.

Pia kuhamasisha na kuwezesha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 – 2030.

Dkt. Biteko ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa na kufanya matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.

Pia, kuendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta vijijini kupitia ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa kipaumbele kingine cha Bajeti ya 2025/2026 ni kutekeleza shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia.

Vilevile kusimamia na kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja kuimarisha matumizi ya gesi asilia (CNG) katika vyombo vya moto.

Ameongeza kuwa kipaumbele kingine ni kuendelea kutekeleza shughuli za kiudhibiti kwa kuimarisha ushiriki wa wazawa katika Sekta ya Nishati pamoja na kuimarisha nguvu kazi na kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi ili kuimarisha tija na ufanisi katika utendaji kazi.

Pia kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na ushiriki wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya Sekta ya Nishati na kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 - 2030 (National Energy Compact 2025 - 2030) kuhusu upatikanaji na uunganishaji wa umeme kwa wananchi.

Awali Dkt.Biteko alilieleza Bunge la Tanzania kuhusu mafanikio mbalimbali ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwemo kukamilika kwa mradi wa kielelezo wa kuzalisha umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) – MW 2,115 na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 160 kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere hadi Chalinze mkoani Pwani.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilika kwa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze na kuingiza umeme unaozalishwa JNHPP kwenye Gridi ya Taifa pamoja na kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida hadi Arusha.

Mafanikio mengine yaliyopatikana katika Bajeti ya 2024/2025 ni kuongezeka kwa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyounganishwa katika Gridi ya Taifa kutoka MW 1,601.84 Mwaka 2020/21 hadi MW 4,031.71 na kukamilika kwa Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze na kuingiza umeme unaozalishwa JNHPP kwenye Gridi ya Taifa.

Pia kukamilika kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na kuunganisha Mkoa wa Kigoma kwenye Gridi ya Taifa na kufanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 58.4 zilizokuwa zinatumika kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya dizeli katika mkoa wa Kigoma.

Katika usambazaji wa umeme vijijini, Dkt. Biteko amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imefikisha miradi ya umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kutoka vijiji 506 vilivyokuwa vimeunganishiwa umeme mwaka 2007 wakati REA inaanzishwa. Pia, kufikisha umeme kwenye vitongoji 33,657 kati ya 64,359 sawa na asilimia 52.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn