logo

SHULE ZA AMALI UFUNDI KUJENGWA PEMBA NA KUSINI UNGUJA-PROF.MKENDA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inatambua kuwa elimu ya amali ni msingi wa maendeleo, kwani inatoa ujuzi wa moja kwa moja kwa vijana, kuwawezesha kujiajiri na kuchangia uchumi wa Taifa.

Waziri Mkenda ameeleza hayo Juni Mosi, 2025, alipokuwa akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya eneo lililotolewa na wananchi wa Kijiji cha Kichokochwe Wete Visiwani Pemba kwa ajili ya kujenga Skuli ya Ufundi, ambapo amewapongeza wananchi kwa hatua hiyo inayochochea maendeleo endelevu.

‘’Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania ameagiza tujenge shule za amali ufundi, kwa upande Zanzibar, shule moja itajengwa Wete Kojani na nyingine itajengwa Kusini Unguja. Vijana watakaomaliza skuli kidato cha Nne watapata cheti cha sekondari na cheti cha ufundi’’ alisema Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika kuboresha miundombinu ya elimu na kuongeza fursa za elimu ikiwemo mikopo ya elimu ya juu, ili kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata elimu bora itakayowakomboa kimaisha.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kojani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Chande, ameishukuru Serikali kuanzisha Ujenzi wa skuli hiyo, na kwamba itawezesha vijana kupata ujuzi kuwawezesha kujiajiri na kushiriki katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

“Skuli hii ya ufundi itakuwa chachu ya mabadiliko kwa maisha ya vijana wetu ambao walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa elimu ya vitendo,” amebainisha Mhe. Chande.

Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Mohamed Nassoro amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hussein Ali Mwinyi, Rais na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuipa kipaumbele sekta ya elimu ikiwemo kuongeza fursa za mikopo kwa Vijana Visiwani Pemba.

"Tunajivunia vijana kadhaa kutoka visiwa vya Pemba ni wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu" Alisema Bw. Nassoro.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn