logo

RAIS DKT.SAMIA MGENI RASMI BUNGE BONANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi tamasha la michezo na burudani lijulikanalo kama Grand Bunge Bonanza, linalotarajiwa kufanyika Jumamosi, Juni 21, 2025 katika viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini, Miyuji jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bunge Bonanza,Mhe.Festo Sanga wakati akizungumza na waandishi wa habari leo June 18,2025 Bungeni Dodoma ambapo amesema lengo la bonanza hilo ni kuimarisha afya za washiriki, kujenga mshikamano, kudumisha mahusiano baina ya taasisi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi kushiriki katika Uchaguzi mkuu.

Tamasha hilo ambalo litahusisha wabunge, taasisi za serikali, wadau wa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla, linatarajiwa kuwa la mwisho katika Bunge la Kumi na Mbili, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe.Sanga amesema michezo mbalimbali ya ushindani itafanyika ikiwemo mpira wa miguu kati ya Bunge na CRDB, mpira wa pete kati ya Bunge na PSSF, kuvuta kamba kwa wanaume kati ya Bunge na Wizara ya Maliasili na Utalii, na kwa wanawake kati ya Bunge na Wizara ya Uchukuzi.

Amesema Bonanza litajumuisha michezo ya furaha kama mpira wa meza, pool table, draft, kucheza bao, kurusha tufe, darts, kukimbia na magunia, kufukuza kuku, kujaza maji kwenye chupa, kushindana kunywa soda, kula chakula kwa kasi, na kuvaa soksi kwa haraka.

"Kutakuwa na mpira wa kikapu kwa wanaume kati ya Bunge na BOT, na kwa wanawake kati ya Bunge na CRDB, huku mpira wa wavu ukichezwa kati ya Bunge na NSSF. Bunge pia litachuana na UDOM katika mpira wa kikapu kwa wanawake"amesema Mhe.Sanga.

Aidha CRDB kama mdhamini mkuu imegharamia vifaa vyote vya michezo vikiwemo medali, jezi, mipira, tracksuit, fulana na kofia kwa washiriki wote ambapo CRDB imeandaa kifungua kinywa kwa washiriki wote pamoja na tafrija ya jioni itakayopambwa na muziki wa dansi, taarabu, ngoma za asili, ushairi na vichekesho vya stand-up comedy.

Hata hivyo kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kutoka CRDB, Tully Mwambapa amesema benki hiyo imekuwa mdau mkubwa wa michezo na jamii kwa ujumla, na imejipanga kuhakikisha Bonanza hilo linakuwa la kipekee na lenye mvuto wa aina yake.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn