MKURUGENZI PURA AFICHUA MAFANIKIO YA ushiriki WA WATANZANIA SEKTA YA MAFUTA NA GESI
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi Charles Sangweni amefichua mafanikio makubwa ya ushiriki wa Watanzania katika sekta ya mafuta na gesi.
.
Mhandisi Sangweni ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika banda la PURA, Mkurugenzi huyo ameeleza kwa kina safari ya mafanikio ya kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa mafuta na gesi amesema.
.
“Wakati tunaanzishwa, kitakwimu ushiriki wa Watanzania kwenye ajira na makampuni ulikuwa chini ya asilimia 55, lakini leo hii tumefikia zaidi ya asilimia 85,” alisema.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yanapimwa kwa kuangalia uwakilishi wa Watanzania katika kampuni zinazojihusisha na shughuli za utafiti na uchimbaji wa mafuta, ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa data za maeneo yenye uwezekano wa kuwepo kwa mafuta na gesi.
Ametolea mfano wa kampeni ya uchimbaji iliyofanyika baharini mwaka 2018, ambapo kwa mara ya kwanza, kati ya wafanyakazi 150 waliokuwemo kwenye meli ya kuchimba mafuta, Watanzania walikuwa 52.
“Kabla ya hapo, tulikuwa tumezoea kuona meli zikiwa zimejaa wataalamu kutoka nje,lakini kupitia kampeni ile, Watanzania walionekana kwa mara ya kwanza kwa wingi, wengi wao wakiwa wamepata uzoefu kupitia miradi ya nyuma na hata kutoka nje ya nchi,” ameeleza
Aidha amesema,kwa sasa maandalizi ya kampeni nyingine ya uchimbaji visima vitatu eneo la Mtwara yanaendelea huku akisema katika kitalu hicho, tayari TPDC inashiriki kwa asilimia 40 ambapo amesema hiyo inaonyesha jinsi kampuni hii ya Tanzania inavyozidi kuwa na ushiriki mkubwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo , PURA inahakikisha kwamba kazi zote zinazoweza kufanywa na makampuni ya Kitanzania zinatolewa kwao.
“Katika kila makampuni 10 tunayoweka kwenye kazi, zaidi ya sita ni ya Kitanzania, hata katika makampuni ya kigeni, nafasi nyingi za uongozi ambazo awali zilishikiliwa na wageni, sasa asilimia 95 ya nafasi hizo zinashikiliwa na Watanzania, pamoja na kwamba ni vita, lakini tunajitahidi kuhakikisha Watanzania wananufaika”amesema na kuongeza kuwa
Kuhusu ushiriki wa PURA kwenye maonyesho ya sabasaba amesema,Mamlaka hiyo ambayo ilianzishwa chini ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, na kuanza rasmi majukumu yake mwaka 2017,tangu wakati huo, imekuwa mshiriki wa kudumu kwenye Maonyesho hayo.
Aidha,amepongeza maendeleo yaliyopatikana katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na mafanikio makubwa katika maonyesho hayo ambapo kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kutembelea banda lao kuliko miaka yote huku wakihoji hasa kuhusu nishati ya kupikia.
Pia amegusia namna wananchi wanavyochukua hatua kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisema hiyo ni ajenda kubwa ya kitaifa na kimataifa inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akisema,kama watendaji wake, wanaendelea kutekeleza maono hayo kwa vitendo na kwamba hawatamuangusha.
PURA inasimamia shughuli zote za utafutaji mafuta katika mkondo wa juu wa sekta ya petroli, na inaendelea kuwa chombo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi zinawanufaisha Watanzania.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

