UPATIKANAJI MAJI SHINYANGA WAFIKIA ASILIMIA 79-RC MHITA
Hali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongezeka kutoka asilimia 63 hadi 79 katika maeneo ya mijini na kutoka asilimia 51 hadi 68 katika maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita leo Julai 14, 2025 jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliolenga kueleza mafanikio ya utekelezaji wa Mkoa huo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uratibu wa Idara ya Habari – MAELEZO na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia programu ya Tumewasikia, Tumewafikia.
Amesema Mkoa huo umepokea zaidi ya shilingi bilioni 113.33 katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya mijini na vijijini hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji ambavyo havikuwa na huduma hiyo 222 kutoka vijiji 162 vya mwaka 2020 hadi Vijiji 384 mwaka 2025.
Aidha, Mhe. Mhita amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jumla ya miradi 64 imekamilika na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini na kuendelea na utekelezaji wa miradi mingine 75 ili kufikia wastani wa asilimia 62.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria katika Vijiji 111 katika maeneo ya Kishapu, Shinyanga na Kahama unaendelea, pia kazi ya usambazaji maji wa Ziwa Victoria kutoka Manispaa ya Kahama kwenda Ushetu kwa gharama ya shilingi bilioni 37.51 inaendelea.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

