logo

BODI MPYA YA WAKURUGENZI WA SHIRIKA LA MZINGA YAZINDULIWA MOROGORO

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax leo tarehe 20 Agosti, 2025, mkoani Morogoro amezindua Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Mzinga, ambayo itakayoongozwa na Luteni Jenerali Mstaafu Balozi Charles Makakala, aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan.

‎.

‎Akizindua Bodi hiyo ya 18 ya shirika hilo, Dkt. Tax amewapongeza wajumbe hao wapya wa bodi hiyo ya shirika la Mzinga kwa kuteuliwa kwao kuliongoza Shirika la Mzinga na ni imani ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan naye pia kuwa Shirika litapiga hatua kubwa zaidi katika kukidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake Septemba 1974.

‎.

‎Waziri Tax amesema hadi sasa hivi shirika hilo limepiga hatua kubwa na nzuri katika miaka ya hivi karibuni ambapo kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao ya Msingi umeongezeka na Shirika limekuwa na miradi mingi yenye tija kwa Taifa na kuleta maendeleo.

‎.

‎"Miradi hiyo ni Ukarabati wa miundombinu ya Shirika, makazi ya watumishi na kuwekeza katika Hospitali ya Mzinga na hivyo kupelekea kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuanzia tarehe 02 Agosti, 2025.

‎.

‎"Natoa Pongezi zangu za dhati kwa Meneja Mkuu wa Mzinga, Brigedia Jenerali Seif Hamisi na timu yake pamoja na bodi iliyomaliza muda wake kwa kujituma,ubunifu na kazi nzuri iliyoleta mafanikio hayo niliyoiyataja" alisema Dkt. Tax.

‎.

‎Aidha, Waziri wa Ulinzi na JKT, ametoa rai kwa bodi mpya aliyoizindua kushirikiana na menejimenti kuyaendeleza mafanikio hayo, na pia amewataka kuongeza jitihada ili uzalishaji na utendaji uimarike zaidi.

‎.

‎“Tuongeze juhudi za uwekezaji katika hospitali yetu ambayo ni tegemeo kubwa si kwa wana Mzinga pekee, bali pia kwa Mkoa wa Morogoro na Taifa, ili kuendana na mahitajio ya sasa na siku za usoni, Niwakumbushe Bodi mpya ya Mzinga jukumu jipya la Kitaifa lililopewa Shirika la Mzinga la kuzalisha zao la msingi kwa ajili ya nchi ya Angola.

‎.

‎“Kazi hii ikikamilika kwa ufanisi na kwa wakati italiletea heshima Shirika letu, kwa ajili hiyo, tuweke mikakati madhubuti ili kutekeleza jukumu hili kwa ufanisi na kwa wakati" alisema Dkt. Tax.

‎.

‎Tukio la Uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Mzinga iliyozinduliwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lilihudhuriwa pia na Wageni mbalimbali toka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Viongozi Chama cha Wafanyakazi wa TUGHE tawi la Mzinga, Wawakilishi toka Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wawakilishi wa wavumbuzi na wabunifu wa shirika hilo.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn