NACTVET YAWATAKA WANAFUNZI WALIOKOSA SIFA KUJIUNGA NA VYUO KUOMBA TENA
Baraza la Taifa la elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (NACTVET) limewataka wanafunzi waliokosa sifa za kujiunga na vyuo kwa mwaka wa masomo 2025/2026 kuomba tena kulingana na kozi zenye sifa zao kabla dirisha la udahili halijafungwa Disemba 12, 2025.
Wito huo umetolewa kufuatia asilimia mbili ya wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vya kati kushindwa kusajiliwa na Nactvet kutokana na kukosa sifa za kujiunga na kozi walizoomba kusomea kwenye vyuo husika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jumatatu Novemba 17,2025, Katibu Mtendaji wa Nactvet Dkt. Mwajuma Lingwanda amesema majina ya wanafunzi walioomba kusajiliwa kupitia vyuo mbalimbali ambavyo vinasajili wanafunzi moja kwa moja kwa vyuo visivyo vya afya kwa mwaka wa masomo 2025/2026 ni 108,109 lakini waliosajiliwa na Nactvet ni 106,022 ambao ni sawa na asilimia 98 ya walioomba huku wengine 2,087 sawa na asilimia mbili wakikosa sifa za kujiunga na vyuo hivyo.
Dkt. Lingwanda amewataka wanafunzi waliokosa sifa za kusajiliwa kuomba nafasi upya kwenye vyuo ambavyo wana sifa za kusoma kabla dirisha la usajili halijafungwa.
“Kuna wanafunzi ambao waliomba kusoma kwenye kozi ambazo hawana sifa za kusomea kwa mfano mtu anaomba kusomea uhandisi lakini hajasomea masomo hayo, hao walikosa sifa za kujiunga na vyuo walivyoomba lakini wanaweza kuomba tena kwenye vyuo ambavyo masomo waliyosoma yanawaruhusu kusoma kozi hizo wafanye hivyo kabla dirisha la usajili halijafungwa,” alisema Dkt. Lingwanda.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

