logo

KITETO YAONGEZA KASI UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE ‎

Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara imeanza rasmi maandalizi ya utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote baada ya kufanyika kwa Kikao Maalum cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) ngazi ya Wilaya kilichoketi Mjini Kibaya tarehe 06 Januari, 2026.

Kikao hicho kililenga kutoa elimu ya awali na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mpango huo muhimu wa Serikali.

‎Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya Msingi na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema, alisema kikao hicho ni hatua ya mwanzo ya kujenga uelewa wa kina kwa viongozi na wadau kabla ya kuanza kwa mfululizo wa vikao maalum vya Tarafa zote saba za Wilaya hiyo kuanzia tarehe 08 Januari, 2026.

‎.

‎Alifafanua kuwa, baada ya vikao hivyo, elimu itaendelea kutolewa kupitia mikutano ya wananchi katika kila kijiji ili kuhakikisha makundi yote yanapata taarifa sahihi kuhusu mpango huo.

‎Mhe. Mwema alibainisha kuwa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya siku 100, ukiwa na lengo la kuwawezesha wananchi wote kupata huduma za afya bila vikwazo na kwa gharama nafuu.

‎Aliongeza kuwa Wilaya ya Kiteto imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanajengewa uelewa wa kutosha kabla ya uzinduzi rasmi wa mpango huo, akisisitiza kuwa jukumu la viongozi ni kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wote.

‎Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kiteto, Ndg. Mufandii Msaghaa, alisema Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ni mkakati wa makusudi wa Serikali wa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, na kuahidi kuwa viongozi wa Wilaya hiyo watahakikisha wananchi wanapata elimu sahihi na yenye tija.

‎Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mhe. Athumani Kilimo, alisema kutoa elimu kwa wananchi ni jambo la msingi katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, akiwataka wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi kushusha elimu hiyo kwa kuzingatia makundi na jamii husika.

‎Kikao hicho kilihudhuriwa pia na wawakilishi wa viongozi wa dini, vyama vya siasa, makundi maalum pamoja na viongozi wa kimila, ambao wote ni wajumbe halali wa Kamati ya Afya ya Msingi ngazi ya Wilaya.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn