logo

HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAPOKEA UGENI WA WAZIRI WA AFYA MALAWI

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema utalii wa kimatibabu unaoendeshwa na hospitali hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kukuza ushirikiano wa utoaji wa huduma za kibingwa kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali.

‎Prof. Makubi ameyasema hayo leo Januari 16, jijini Dodoma, mara baada ya hospitali hiyo kupokea ugeni wa Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira kutoka nchini Malawi, aliyefika kujionea namna Hospitali ya Benjamin Mkapa inavyotoa huduma za afya na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya afya kati ya nchi hizo mbili.

‎Amesema ziara hiyo imelenga kujifunza namna sekta zilizo chini ya Wizara ya Afya ya Serikali ya Tanzania zinavyofanya kazi, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, kupata fursa za matibabu katika hospitali za Tanzania pamoja na kuimarisha ushirikiano wa afya baina ya nchi hizo.

‎Prof. Makubi amesema tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa mwaka 2015, takribani wagonjwa 400 kutoka mataifa mbalimbali wamepatiwa huduma za matibabu ya kibingwa, ikiwemo upandikizaji wa figo, upasuaji wa moyo na upandikizaji wa uroto.

‎Kwa upande wake, Waziri wa Afya na Usafi wa Mazingira wa Jamhuri ya Malawi, Mhe. Madalitso Baleyi, amesema wataalamu wa afya kutoka Malawi na Tanzania wataendelea kubadilishana uzoefu hususan katika huduma za afya ya uzazi pamoja na usambazaji wa vifaa tiba.

‎Mhe. Baleyi ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa utoaji wa huduma za kibingwa zenye viwango vya juu na kuvuka mipaka ya kitaifa, akisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha sekta ya afya.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn