MUHIMBILI YAPANDIKIZA FIGO WATU WANNE WANNE KWA NJIA YA TUNDU DOGO
Madaktari bingwa wa upandikizaji figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wanne kwa kutumia teknolojia ya upasuaji wa njia ya tundu dogo (laparoscopic surgery), hatua inayotajwa kuongeza ubora wa huduma na kuharakisha uponaji kwa wagonjwa pamoja na wachangiaji wa figo.
Teknolojia hiyo ya kisasa inayotumia vifaa maalum vya upasuaji imewezesha madaktari kufanya upasuaji kwa usahihi zaidi bila kufungua sehemu kubwa ya mwili, hali inayopunguza maumivu, kupunguza upotevu wa damu pamoja na muda wa mgonjwa kukaa hospitalini baada ya upasuaji.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Bingwa wa Upandikizaji Figo hospitalini hapo Dkt. Jonathan Mgumi ameeleza kuwa:
.
"Matumizi ya njia hii yameongeza usalama kwa wachangiaji wa figo kwani hupata nafuu kwa haraka na kurejea katika shughuli zao za kawaida mapema zaidi ikilinganishwa na upasuaji wa kawaida" alisema Dkt.Mgumi.
Ameongeza kuwa hospitali itaendelea na matumizi ya teknolojia za kisasa katika huduma za upandikizaji figo ili kuimarisha huduma za kibingwa na bingwa bobezi nchini, sambamba na kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kutafuta huduma hizo nje ya nchi.
Kwa upande wake Dkt. Emanuel Minja ambaye ni Mtanzania anayefanya kazi nchini Marekani na mtaalam bobezi wa upasuaji wa upandikizaji figo kwa njia ya tundu dogo, aliyeongoza jopo la madaktari wa Muhimbili katika utekelezaji wa upasuaji huo wa kisasa, ameeleza kuwa ujio wa teknolojia hiyo umeongeza ufanisi wa huduma za upandikizaji figo nchini kwa kuwezesha upasuaji kufanyika kwa usahihi mkubwa zaidi huku ukipunguza madhara na muda wa wagonjwa pamoja na wachangiaji kurejea katika hali zao za kawaida.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

