BODI ZA USULUHISHI WA NDOA ZIJIKITE KWENYE MARIDHIANO
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, Mhe. Apolinary Mugarula, amesema wajumbe wa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa hawapaswi kujiona kama mahakimu wa kutoa hukumu bali wawe wasuluhishi wanaosaidia wanandoa kufikia muafaka kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.
Mhe. Mugarula amesema hayo wakati akifungua mafunzo kwa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa Wilaya ya Biharamulo yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe hao katika kutatua migogoro ya kifamilia kwa amani na haki.
Amesisitiza kuwa jukumu kuu la bodi hizo ni kutumia njia mbalimbali za maelewano ili kusaidia pande zinazohusika kurejesha amani ndani ya familia badala ya kuongeza migogoro.
“Nichukue nafasi hii kusisitiza kuwa wajumbe wa bodi si mahakimu. Ninyi ni wasuluhishi. Jukumu lenu si kutoa hukumu, bali kutumia kila njia zinazowezekana kusaidia pande mbili kufikia muafaka kwa njia ya mazungumzo na maridhiano,” amesema Mugarula.
Aidha, amewataka wajumbe hao kuzingatia maadili ya kazi yao ikiwemo kutunza siri za wanandoa, kutokuwa na upendeleo, kuendesha usuluhishi kwa haki na heshima pamoja na kujiepusha na rushwa.
Katika hatua nyingine, Mugarula amesema serikali inatambua mchango wa wadau mbalimbali katika kuimarisha utendaji wa bodi hizo, wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Mahakimu, Wanasheria, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Zerafina Boaz Gotora, amesema bodi hizo zina nafasi muhimu katika kulinda na kuimarisha taasisi ya ndoa ambayo ni msingi wa familia na jamii imara.
Amesema kupitia mafunzo hayo, washiriki wanatarajiwa kupata maarifa na ujuzi utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa katika kutatua migogoro ya ndoa kwa njia ya maridhiano.
Nao baadhi ya wajumbe wa Bodi za Usuluhishi wa Ndoa waliohudhuria mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata itasaidia kuinufaisha jamii kwa kupunguza, na hata kumaliza, migogoro ya ndoa inayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya mitaani.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

