MAJAJI NA WATAALAMU WANOLEWA KUELEKEA MASHINDANO YA KITAIFA YA UJUZI 2026
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeendesha mafunzo maalum kwa wataalamu na majaji watakaoshiriki katika Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi 2026 yanayotarajiwa kufanyika jijini Tanga mwezi Juni, 2026.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza tarehe 15 Mei, 2026 jijini Dodoma, yakilenga kuwawezesha wataalamu hao kupata uelewa wa kutosha kuhusu usimamizi wa mashindano ya ujuzi kwa kuzingatia taratibu, kanuni, miongozo, haki, uwazi, pamoja na viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa NACTVET, Dkt. Jofrey Oleke, amesema mashindano ya ujuzi ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhamasisha maendeleo ya ujuzi miongoni mwa vijana kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, kwa lengo la kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika masuala ya ujuzi ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku mashindano hayo yakitarajiwa kuongeza hamasa kwa vijana kushiriki katika mafunzo ya ufundi na ufundi stadi pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vya TVET na sekta ya viwanda.
“Mashindano haya yanalenga kuibua vipaji, kukuza ubunifu na kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika viwango vya kimataifa,” amesema Dkt. Oleke.
Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi yataanza katika ngazi ya vyuo, kanda na baadaye kitaifa, ambapo washindi watapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kimataifa ngazi ya Afrika na hatimaye dunia.
Fani zitakazoshindaniwa ni pamoja na urembo, uwekaji wa vigae ukutani na sakafuni, ufundi umeme, uhandisi wa mitambo, uchomeleaji na uungaji wa vyuma, mekatroniki, upishi, huduma za chakula na vinywaji, ushonaji, ubunifu na teknolojia ya nguo pamoja na mtandao wa vitu (IoT).
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

