logo

MHE.MWANAIDI:TUTAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA KWA MAAFISA USTAWI WA JAMII

Serikali itaendelea kuboresha mazingira, miundombinu na Huduma kwa Maafisa Ustawi wa Jamii ili wafanye kazi kwa ufanisi.

Akifunga mkutano wa mwaka wa kiutendaji wa Maafisa Ustawi wa Jamii, Septemba 7, 2023 Naibu Waziri wa @maendeleoyajamii Mhe. @mwanaidi_ali_khamis amesema Maafisa hao wana dhamana kubwa kuhakikisha usalama na amani ndani ya jamii.

"Ajenda hii ni muhimu na imebebwa kwa uzito na viongozi wetu wa kitaifa hususani Mhe. Samia Suluhu Hassan, ndio maana aliunda Wizara hii kwa sababu anajua changamoto, malengo, matatizo ya Watanzania hivyo Maafisa mliopo hapa mtakuwa mabalozi wazuri kwa wananchi, muwapokee, mtatue matatizo yao, wajue kwamba Serikali yao ipo inafanya kazi." amesema Mhe. Mwanaidi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu @maendeleoyajamii Dkt. Seif Shekalaghe amesema Maafisa Ustawi wa Jamii ni muhimu sana kwa jamii kwani matatizo mengi yanayotokea hasa ukatili wa kijinsia yanatokana na uwepo wa matatizo ya kisaikolojia hasa Afya ya akili.

"Sisi Makatibu Wakuu na ninyi Maafisa Ustawi wa Jamii ndio watekelezaji wa mambo yote kwa wananchi naamini tukionesha mshikamano nawahakikishia kuwa malengo yetu ya kuwahudumia wananchi yatakuwa yametimia" alisema Dkt. Shekalaghe

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Dkt. Wilson Charles amewaambia Maafisa Ustawi wa Jamii hao kuwa Ofisi hiyo itashirikiana na Mamlaka nyingine kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo uhaba wa Maafisa na vitendea kazi katika kuwahudumia wananchi.

Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Ustawi wa Jamii umeshirikisha kutoka Wizara, Mikoa Halmashauri na Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi ukiwa na kauli mbiu isemayo: Malezi Makuzi na Afya Bora ya Akili ni Jukumu letu sote.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn