logo

WIZARA YA ELIMU YATANGAZA WASHINDI TUZO ZA WATAFITI WALIOCHAPISHA KATIKA MAJARIDA YA HADHI YA JUU KIMATAIFA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imetangaza watafiti 47 kutoka taasisi za elimu ya juu za umma na binafsi, ambao wameshinda tuzo kwa kuchapisha matokeo ya utafiti waliofanya kwenye majarida yenye hadhi ya juu kimataifa katika nyanja za afya, sayansi shirikishi, sayansi asilia na hisabati.

Akizungumza leo jijini Dodoma katika hafla ya kutangaza washindi hao, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kila chapisho lililofikia vigezo, mhusika atapata Sh50 milioni, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kuongeza hamasa na morali kwa watafiti katika maeneo ya sayansi na teknolojia.

“Kila chapisho lililoshinda limetengewa Sh50 milioni. Tunataka wahadhiri wetu wawekeze muda, akili na nguvu katika kufanya tafiti ambazo zitatatua changamoto katika jamii na kuchangia maendeleo ya Taifa.

.

“Serikali inaona haja ya kuwawezesha wanasayansi wetu katika utafiti; tunachokifanya ni kidogo lakini kinatuma salamu. Tunataka mtafiti aweze kuchuma maisha yake kutokana na utafiti.” alisema Mkenda.

Amesema fedha walizopata zitachagiza wengine kujikita kwenye utafiti wenye tija kwa Taifa na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

“Tunataka watafiti wajikite kwenye utafiti na si kufanya biashara ili wapate fedha. Tunataka waende kwenye majarida hayo, ili utafiti wao ujiuze kimataifa na kuwezesha kujikwamua kiuchumi,”amesema Mkenda.

Wakati huohuo, Waziri amezindua awamu ya pili ya uwasilishaji wa machapisho yaliyochapishwa kati ya Julai Mosi 2022 na Mei 31, 2023 katika nyanja za sayansi ya kilimo na mifugo, uhandisi na Tehama. Alitaja tarehe ya mwisho kuwasilisha machapisho hayo ni Oktoba 31, 2023.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23, bajeti iliyopitishwa ilikuwa Sh bilioni moja, sasa tumetumia Sh 500 milioni katika nyanja za afya, sayansi shirikishi, sayansi asilia na hisabati. Tunafungua tena dirisha ili kuchukua nyanja tulizoacha ambazo machapisho yake yamo ndani ya kipindi hicho ,”amesema.

Amesema kwa wale ambao machapisho yao yalianza kuchapishwa Juni Mosi 2023, dirisha hilo litatangazwa baadaye.

@wizara_elimutanzania

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn