logo

TANZANIA YASAINI MIKATABA 2 YA MSAADA KWA AJILI YA KUNUSURU KAYA MASKINI AWAMU YA PILI(PSSN II)

Serikali ya Tanzania imesaini mikataba miwili ya msaada yenye thamani ya dola za Marekani milioni 20.3 sawa na shilingi bilioni 50.13 kwa ajili ya kunusuru kaya masikini awamu ya pili (PSSN II).

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba alisema msaada huo umetolewa na Serikali ya Uswisi dola za Marekani milioni 18 na Euro milioni 2.2 sawa na dola za Marekani milioni 2.3 zimetolewa na Serikali ya Ireland.

"Kiasi cha misaada kilichosainiwa leo ni mwendelezo wa misaada mingine iliyopokelewa kutoka kwa serikali hizi mbili ambapo misaada ya kipindi cha nyuma kwa mpango huu wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili ilikuwa faranga za Uswisi milioni 15.72 sawa na dola za Marekani milioni 17.1 kutoka serikali ya Uswiss na Euro milioni 2 sawa na dola za Marekani milioni 2.1 kutoka serikali ya Ireland. ," alisema Dkt. Mwamba.

Alisema misaada hiyo imewezesha serikali kufanya kazi yao kuwa rahisi katika kuleta maendeleo kwa watanzania wote.

Aidha, PSSN II inaendana na Dira ya Tanzania ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo inatoa mwelekeo wa juhudi za kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii hadi kufikia mwaka 2025.

"Dira hii kwa sasa inatekelezwa kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ," alisema Mwamba.

Alisema kwamba pia misaada hii pia inaendana na lengo la kwanza la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambalo linalenga kuondoa umaskini wa aina zote ifikapo mwaka 2030, na ajenda ya Afrika ya mwaka 2063 ambayo inalenga kuwezesha mpango wa Afrika kufikia ukuaji jumuishi na endelevu wa uchumi na maendeleo ifikapo mwaka 2063.

Alisema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umewezesha wanafunzi kutoka Kaya maskini kupata elimu ya sekondari na elimu ya Juu. Mwaka 2022 wanafunzi 2,950 kutoka kaya maskini walipata mkopo wa asilimia 100 kutoka bodi ya mikopo ya Elimu ya juu chini ya msaada wa PSSN II.

Aidha alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeanza kuimarika ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2023 ukuaji ulikuwa ni asilimia 5.6

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn