SERIKALI, JUKWAA LA MASHIRIKA YASIYO YA SERIKALI WAWAKUMBUKA WAHITAJI
Serikali pamoja Wadau kutoka Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, wametoa vitu mbali mbali ikiwa ni sehemu ya sadaka kwa ajili ya wahitaji katika kituo cha kulelea watoto cha Matumaini kilichopo Miuji jijini Dodoma Oktoba 03,2023.
Wakati wa zoezi hilo, Mwakilishi wa Serikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mussa Sang'anya ambaye ni Msajili Msaidizi amekemea vikali vitendo vya ukatili na kuitaka jamii kuungana kwa pamoja kupiga vita ukatili.
Sang'anya amesema Serikali inaendelea na juhudi za kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kwa kuandaa mazingira salama yatakayo wawezesha kukua bila kupata changamoto.
“Serikali inaendelea kuja na afua mbalimbali zitazohakikisha watoto wa taifa hili hususani wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi wanaweza kuishi katika mazingira mazuri yatakayo wawezesha wao kukua na kustawi vyema” amesema Musa.
Akitoa Salaam za Kituo, Mkuu wa Kituo hichi Sr. Aurea Kyala amesema ukatili dhidi ya watoto bado umekithiri ndani ya jamii hivyo juhudi kubwa bado zinatakiwa kuwekezwa na jamii kwaujumla ili kukabiliana na changamoto hii.
“Jamii inahitaji kubadili mtazamo wa kifikra kwani bado kuna changamoto kubwa ya kuwanyanyasa watoto hasa wale ambao wazazi wao wamefariki kwa ugonjwa wa UKIMWI kwani wanawafanyia ukikatili wa hali ya juu unaoishia kuwafanya watoto hao kujiona dhaifu “amesema Sr.Aurea.
Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Mwakilishi wa NACONGO Mkoa wa Dar Es Salaam Jane Magigita ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kusaidia watoto walioko katika makao hayo na makosa mengine nchini waweze kupatiwa huduma za msingi ikiwemo malezi na makuzi yao.
Msaada huo ambao umetolewa Oktoba 03, 2023 ni pamoja na sukari, unga wa ngano, sabuni za kufulia na kuogea, nguo za watoto, kanda mbili pamoja na kufanya Malipo ya umeme wenye thamani ya shilingi za kitanzania laki tano.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

