WAJAWAZITO WATAKIWA KUZINGATIA LISHE KUEPUKA KUJIFUNGUA WATOTO NJITI
Kinamama wajawazito wametakiwa kuzingatia lishe bora ili kuepuka kujifungua watoto njiti ambapo Takribani wakinamama 220,000 kati ya milioni 2 ambao hujifungua kila mwaka sawa na asilimia 11 hupata watoto waliozaliwa kabla ya wakati wao (watoto njiti) hali inayosababisha vifo vya watoto hao.
Akizungumza jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya siku ya watoto Njiti inayoadhimishwa kila ifikapo Novemba 17 ,Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika amesema takribani watoto wapatao 50,000 wenye umri chini ya Siku 28 hufariki hapa nchini, ambapo watoto 13,500 kati yao sawa na asilimia 27% kutokana na changamoto za kuzaliwa kabla ya wakati.
"Watoto kuzaliwa kabla ya wakati inachangia sana kwenye Vifo vya watoto wanaofariki chini ya siku 28, idadi hii ni kubwa, wapo watoto pia wanazaliwa hapa wakiwa na gramu 700 hata kilogramu hawajafika,Lakini wameweza kuhudumiwa kupona na kufikia hatua ya kuruhusiwa na kuondoka kwenda majumbani, niendelee kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha upatikanaji wa miundombinu bora ikiwemo vifaa tiba, dawa na watumishi wenye mafunzo maalum" alisema Chandika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Watoto katika hospitali hiyo, Dkt.Julieth Kabengula, amesema sababu zinazopelekea mwanamke kujifungua mtoto kabla ya wakati ni pamoja na lishe duni kwa mama mjamzito,shinikizo la damu,kisukari nk.hivyo amewataka wakina mama wajawazito wote nchini kuhakikisha wanafanya maandalizi ya miili yao kabla ya kupata mimba.
Idadi ya watoto wanaopewa rufaa kwenda katika Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kuongezeka ambapo kwa mwaka 2021 walihudumia watoto 25 waliozaliwa kabla ya wakati, na mwaka huu wamehudumia watoto wapatao 108.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

