logo

WAZIRI MKUU MAJALIWA: VIONGOZI JESHI LA MAGEREZA WEKENI MKAKATI WA KUONGEZA UZALISHAJI MALI

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amewataka askari wote waliohitimu mafunzo ya Uongozi wa Juu na Daraja la Pili wa Jeshi la Magereza kutambua kuwa kupandishwa vyeo ni kuongezewa majukumu mengine hivyo kila askari anatakiwa kujipanga vyema ili kukabiliana na majukumu mapya atakayopewa.

Mhe.Majaliwa ameyasema hayo leo Disemba 15,2023 alipokuwa katika viwanja vya Jeshi la Magereza akifunga Mafunzo ya Uongozi wa Juu na Daraja la Pili kwa Askari wa Jeshi la Magereza (TCTA Ukonga) Jijini Dar Es Salaam.

.

Amesema kufaulu kwao katika mafunzo hayo ni ishara kwamba wamepata maarifa, ujuzi, uzoefu na mbinu bora zitakazowawezesha kumudu majukumu yao, hivyo kila mmoja akatumie stadi alizozipata kupitia mafunzo katika kuwasimamia watumishi na jukumu la kuwarekebisha wahalifu waliopo Magerezani.

"Ninatambua kuwa kujifunza ni kitu kimoja na kutumia maarifa ni kitu kingine. Hivyo basi wahitimu wote mkazingatie mafunzo mliyoyapata ili yakawe chachu katika kuboresha utendaji kazi wa majukumu yenu ya kila siku" Alisema Majaliwa.

.

Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi wa Jeshi la Magereza kuweka mkakati wa kuongeza uzalishaji mali pamoja na kuweka usimamizi wa kutosha wa rasilimali za magereza, na pia ubora wa miradi watakayotekeleza iwiane na thamani halisi ya fedha inayotolewa na Serikali.

.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya maboresho kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa fedha kwa ujenzi wa majengo ya magereza katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo imetenga bilioni 2.769 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Magereza" Alisema.

.

Waziri Mkuu pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuweka mikakati ya kuongeza matumizi ya TEHAMA kwa kuwapeleka mafunzo maafisa na askari wao ili vyombo vyetu viende na wakati na kumudu mabadiliko na changamoto zinazotokana na kasi ya ubunifu na matumizi ya teknolojia za kisasa.

.

Aidha,Majaliwa ametoa pongezi kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhani kwa kuwezesha utekelezaji wa mpango wa mafunzo ya kuwajengea uwezo na weledi maafisa katika kutekeleza majukumu ya kuwapokea, kuwahifadhi, kuwalinda na kuwarekebisha wahalifu wanaoletwa Magerezani.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn