logo

DKT.BITEKO AGAWA MITUNGI YA GESI NA MAJIKO BANIFU KWA WAJASIRIAMALI DAR ES SALAAM

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko amesema kuwa safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza rasmi nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa wananchi na hasa kina mama Tanzania wanahama kutoka matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi kwenda kwenye nishati iliyo safi na salama.

Amesema hayo leo Machi 07,2024 wilayani Temeke Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi na majiko banifu kwa wajasiriamali katika Soko la Temeke Stereo na Mbagala- Zakhem.

“Nataka niwaeleze kuwa, safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza katika wiki hii ambayo tunasherehekea siku ya Wanawake Duniani kwa sababu tunafahamu kwamba Mwanamke ni mwathirika mkubwa nishati isiyo safi ya kupikia na wanapata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kifua, kubakwa na kutumia muda mrefu kutafuta kuni hivyo Serikali imeona kuwa ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ili kumwezesha mwanamke kupata nishati safi na kwa gharama nafuu.” amesema Dkt.Biteko.

Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia siyo tu kwa Tanzania bali Afrika nzima na ulimwenguni; na hii ilithibitika wakati akizindua Programu ya Nishati safi ya kupikia itakayosaidia Wanawake Barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme (AWCCSP) katika Mkutano wa Cop 28 Dubai ambayo imeungwa mkono na wadau mbalimbali hivyo kama nchi lazima iwe na mpango maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa zoezi hilo la ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko banifu halitaishia Dar es Salaam bali ni endelevu na litafanyika katika mikoa mbalimbali nchini ili wananchi katika maeneo yote wahamasike kutumia nishati safi ya kupikia.

Dkt.Biteko ametoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wa Dini,Serikali,Jadi na makundi mengine kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia huku akisisitiza kuwa ajenda hiyo isiwe ya Serikali pekeyake, ambapo pia ameomba wadau zaidi wajitokeze kuungana na Serikali katika suala hilo kama ilivyo kwa kampuni ya Oryx ambayo imeonesha kwa vitendo kuwa inaiunga mkono Serikali kwenye nishati safi ya kupikia.

Aidha, amezitaka Taasisi kama vile Shule, Magereza na Hospitali watumie gesi kwenye matumizi ya kupikia na kuanza kubadilisha mifumo ya matumizi ya kuni kwenda kwenye Gesi ili kufanikisha ajenda ya Serikali ya Matumizi ya Nishati safi ya kupikia.

.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga amemshukuru Dkt.Biteko kwa maono yake ya kuhuisha azma na maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia na pia kuendeleza kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn