logo

MRADI WA MMT WA NELSON MANDELA WAFIKIA KAYA 2,874

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kupitia Mradi wa Mycotoxins Mitigation Trial (MMT) kwa kushirikiana na Chuo cha Cornell umefanikiwa kuzifikia kaya 2,874 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuanzia Juni 2017 hadi Aprili 2024.

Hayo yamesemwa na Profesa Mshiriki na Mtafiti kutoka taasisi hiyo Prof. Neema Kassim katika warsha ya wiki moja ya mapitio ya jarida la kutoa mrejesho wa utafiti wa mradi huo ambao umejikita katika utafiti wa ubora na usalama wa chakula, na ukuaji wa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 18 , uliofanyika April 2 hadi 5, 2024 Mkoani Manyara.

Profesa Neema anaeleza kuwa wakati wa utafiti kulikuwa na makundi mawili ambayo yalipewa chupa za chai kwa ajili ya kuhifadhia chakula cha watoto, pamoja na mafunzo ya usafi binafsi, maji na mazingira (WASH), unyonyeshaji na ulishaji wa watoto wadogo.

Anazidi kueleza kuwa kundi la kwanza la majaribio lilipewa unga wa uji wenye mchanganyiko wa mahindi 4; karanga 1; ulioandaliwa na mradi kwa kuzingatia ubora na usalama na kundi la pili la udhibiti lilipewa mafunzo ya namna sahihi ya kuandaa unga wa uji wenye mchanganyiko wa mahindi 4; karanga 1; kwa kutumia mahindi na karanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt.Omari Nkullo amesema mrejesho wa utafiti huo utawapa mwongozo wa namna sahihi ya kuweka mikakati ya kutoa elimu kwa jamii ya Kongwa juu ya namna bora ya kupunguza sumukuvu kwenye mahindi na karanga wakati wa kuandaa chakula cha watoto na familia kwa ujumla.

Dkt.Nkullo ameishukuru Taasisi ya Nelson Mandela,Chuo cha Cornell kwa kushirikiana na Wilaya ya Kongwa kufanya utafiti huo muhimu kwa jamii.

Naye Rosemary Kayanda, mwanafunzi wa Shahada ya uzamivu katika Taasisi ya Nelson Mandela amesema kuwa, kwa kiasi kikubwa utafiti huo ulihusisha mazao ya mahindi na karanga ambayo yalionekana kutumika zaidi katika kuandaa uji wa watoto na ugali kwa familia.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn