logo

KINANA AWATAKA VIONGOZI WA CHAMA NA SERIKALI KWENDA KUJIFUNZA KAZI BUTIAMA "AMPIGIA SALUTE MBUNGE SAGINI"

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndg. Abdulrahman Kinana amempongeza Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM na kuitangaza wilaya Butiama sehemu ya mfano ambayo viongozi mbalimbali wa chama na serikali wataitembelea na kujifunza.

Kinana ametoa pongezi hizo Aprili 15,2024 wakati alipokuwa akihotubia Kikao cha Halmashauri Kuu na Mabaraza ya Jumuiya CCM wilayani Butiama katika Ukumbi wa Kanisa Katoliki uliopo kijijini Butiama Kata ya Butiama ambapo amewataka wajumbe wa CCM waendelee kumuamini Mbunge Sagini kwa awamu nyingine ili azidi kuipendezesha Butiama kama ilani inavyomuelekeza.

"Nikiulizwa wilaya ya mfano ya Chama Cha Mapinduzi kwa utekelezaji wa ilani mshikamano wa taasisi zote, Chama, halmashauri na serikali sitosita kusema ni Butiama hivyo niwapongeze pia wajumbe wa CCM Butiama kwa kumpitisha Mhe.Jumanne Sagini bila kupingwa katika uchaguzi uliopita kwani anazungumza kwa vitendo si kwa kelele, anashawishi hatishi, anaunganisha hagawanyi na anajiamini haogopi hii ni kwa sababu amekaa kwa muda mrefu serikalini ndio kumemfanya afanye mambo makubwa ya kimaendeleo hapa Butiama kwani anajua fedha zinapopatikana,"

"Pia nimpongeze Mkuu wa Wilaya Mhe. Moses Kaegele kwa kazi nzuri anayofanya Butiama ingawa bado kijana ila hajikwezi kutokana na cheo chake kama viongozi wengine vijana wanaopata vyeo kama vyake wanaanza kusumbua watu sambamba na Mkurugenzi wa Halmshauri, Mwenyekiti wa Halmashauri, Madiwani na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya hii hakika mnafanya kazi kwa pamoja na kujituma ndio chanzo cha maendeleo tunayoyaona," alisema Kinana

Aidha,Kinana amewashauri wajumbe wa CCM kuwa kama wanataka Jimbo la Butiama liendelee kupaa kimaendeleo wasithubutu kumpoteza Mhe. Jumanne Sagini katika Awamu nyingine kwani miaka mitano haimtoshi kuwafanikishia maendeleo hivyo wamuache kwa Awamu nyingi zaidi pia iwe hivyo hata kwa madiwani anapokesea aitwe aonywe asitangazwe hadharani ili kumuharibia kwa wapiga kura wake.

Hata hivyo Kinana amepongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kila wilaya anaacha alama kama alivyotoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwl. Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia ambacho kilikaa kwa muda mrefu bila kuanza na Awamu zilizopita hazikuchukua hatua ila alipoingia yeye mchakato ukaanza haraka.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn