logo

POSTA YAKABIDHIWA PIKIPIKI 22,CCTV CAMERA 10,SCANNER 127, KOMPYUTA 10 KUTOKA UPU

Mkurugenzi wa Biashara Mtandao (E-Commerce) na huduma za Fedha na Uwakala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati namba 2 ya Baraza la Uendeshaji la Umoja wa Posta Duniani (UPU) Bw.Constantine Kasese kwa niaba ya Postamasta Mkuu, amewaasa watendaji wa Shirika la Posta Tanzania kuhakikisha wanatoa huduma kwa ufanisi kama inavyohitajika na wateja.

Kasese ameyasema hayo tarehe 16 Aprili,2024 katika Makao Makuu ya Posta jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi pikipiki 22 zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 145 pamoja na kompyuta mpakato (Laptop) 6, kompyuta za mezani (Desktop) 10, Printer 4, CCTV camera 10, vifaa vya mawasiliano (Network equipment) 3, scanner 127 kutoka Umoja wa Posta Duniani (UPU).

Vifaa hivi vimelenga kurahisisha utoaji wa huduma za Posta nchini hasa katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi sambamba na maeneo yaliyokumbwa na majanga/maafa yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambavyo vimetolewa chini ya mradi wa DRM (Disaster & Risk Management) wenye lengo la kutoa huduma za Posta zenye ufanisi katika maeneo mbalimbali yenye majanga.

Akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo, Bw.Kasese ametoa wito kwa wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kuhakikisha wanazitumia vifaa hivyo kwa weledi kama ilivyokusudiwa kuongeza ufanisi ili zikaongeze mapato sambamba na kuwafikishia wananchi huduma kwa wakati ikizingatiwa uwepo wa Mfumo wa Anwani za Makazi unaorahisisha kumfikia mteja mpaka mahali alipo.

Aidha, Bw. Kasese ameushukuru Umoja wa Posta Duniani (UPU) kwa kuona umuhimu wa kuliwezesha Shirika la Posta Tanzania kupata vifaa hivyo huku akiahidi kuhakikisha vifaa hivyo kutumika kwa ufanisui kama vilivyokusudiwa ili kuwapatia wananchi huduma stahiki mpaka mahali walipo sambamba na mahitaji yao.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn