WANANCHI WAHIMIZWA KUHAMA MAENEO HATARISHI
Wananchi wamehimizwa kuendelea kuchukua tahadhari na kuondoka katika maeneo hatarishi yenye viashiria vya kuathiriwa na maafa ili kuendelea kuwa na jamii salama na tulivu hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Hayo yameelezwa hii na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na maafa ya mafuriko yaliyotokea tarehe 25 Aprili, 2024 katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo Kata ya Saranga, Mji Mpya na Kimochi ziliathiriwa na maafa hayo.
Dkt.Yonazi ametoa rai kwa wananchi kuzingatia taarifa zinazotolewa na Serikali pamoja na kuendelea kuchukua tahadhari za mapema ili kuendelea kujilinda na kuendelea kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya maafa.
“Serikali itaendelea kukabiliana na maafa mbalimbali nchini kwa kuendelea kutoa elimu juu ya namna ya kujiandaa na kukabili maafa ili kuondokana na madhara yatokanayo na maafa pindi yanapotokea,” alisema Dkt.Yonazi.
Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye dhamana ya masuala ya menejimenti ya maafa hivyo itaendelea kuratibu kwa weledi na kuyafikia malengo kama inavyotakiwa.
Aidha,alihimiza uongozi wa Mkoa kuendeleza juhudi katika kuelimisha umma kuhusu masuala ya maafa pamoja na kuendelea kuwatumia wataalamu wa masuala ya Ustawi wa jamii lengo ni kutoa huduma za kisaikolojia kwa waathirika wa maafa hayo ili kuondokana na madhara waliyoyapata na kuweza kurejea katika hali zao na kujiletea maendeleo yao ya kila siku.
“Tutaeendelea kushirikiana na mkoa wa Kilimanjaro ili kuona hatua bora za urejeshaji wa hali na kipekee niendeleee kuupongeza uongozi wa Mkoa huu kwa hatua mlizochukua toka maafa yalipotokea niwasihi kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya majanga na maafa,”alisisitiza.
Akitoa taarifa ya hali ya maafa kwa Katibu Mkuu huyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bi.Mwajuma Nasombe amesema kuwa, maafa hayo ya mafuriko yaliathiri Kata mbili ikiwemo ya Saranga na Mji Mpya zilizopo Manispaa ya Moshi na kusababisha athari kwa Kaya 283 zenye jumla ya watu 1195.
“Jumla ya nyumba 51 na kifo cha mkazi mmoja kilitokea katika maeneo ya Mji Mpya ambapo nyumba 35 zilibomoka kuta, nyumba 15 kuvunjwa na maji pamoja na nyumba moja kubomoka kabisa”alieleza.
Aidha,alisema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya tathimi ya kujua maeneo yaliyoathirika, kutoa huduma na misaada ya kibinadamu, kutenga maeneo ya maalum ya kuwahifadhi (kambi maalumu) ili kuwapatia mahitaji waathiriki wa maafa hayo.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

