logo

MAKONDO ATAKA UMAKINI DAWATI LA HUDUMA ZA KISHERIA

Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha Dawati Maalum la huduma za kisheria katika ofisi za wizara hiyo kwa lengo la kutatua huduma za wateja wenye malalamiko juu ya huduma za kisheria zinazotolewa katika mifumo mbalimbali ya utoaji haki.

Akizungumza na baadhi ya watumishi wa wizara wanaotoa huduma katika dawati hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Gasper Makondo alisema dawati hili litarahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi hasa wale wanaofika wizarani kwa ajili ya msaada zaidi.

Aidha Bi.Makondo aliongeza kuwa wananchi wana imani kubwa na serikali hasa kupitia kampeni hii ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia hivyo kila mtumishi ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa uadilifu kwa lengo la kuwasaidia wananchi hasa wale wasioukuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili na hatimaye watimize maono ya Rais Samia juu ya wananchi wote kupata haki.

“Wapo watu wana matatizo na wanahangaika kupata msaada wa kisheria lakini hawajui waanzie wapi, wafanye nini ili kupata huduma hii. Tumeanzisha dawati hili ili mteja atakayefika wizarani aweze kupata huduma bila ya kupoteza muda mrefu kuzunguka maofisini hasa kwa changamoto ambazo nyingi zinahitaji uelewa zaidi. Hivyo hakikisheni mnatoa huduma kiuweledi ili tuweze kuwasaidia wananchi” alisema Bi.Makondo.

Aidha,Katibu Mkuu huyo alitoa rai kwa watumishi wanaowapokea wateja wanaofika wizarani hapo kwa ajili ya huduma kuhakikisha kuwa kuwa wanatumia lugha nzuri, busara na kutoa huduma ndani ya muda mfupi kwani wananchi wengi wanaofika wizarani wanatoka kila pembe ya nchi na wakifika wizarani wanakuwa na tumaini kuwa matatizo yao yatapatiwa ufumbuzi.

“Ninapokea wananchi wengi kila siku na wapo wanaotokea maeneo mbali kabisa wanasafiri kwa tabu ila wakiamini kuwa wakifika hapa wizarani wanaamini wameleta changamoto zao sehemu sahihi. Sasa tunapowahudumia tukumbuke gharama na muda walioutumia mpaka kufika hapa badala ya kuwapa majibu mepesi ambayo hayawasaidii katika changamoto zao.” aliongeza Bi.Mary Makondo.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn