logo

WIZARA YA FEDHA YAOMBA KUIDHINISHIWA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI SH.TRILIONI 44.19

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. @mwigulunchemba (Mb), ameliomba Bunge la Tanzania, kuiidhinishia Wizara yake makadirio ya mapato na matumizi ya sh. tril. 44.19, kati ya makadirio ya sh. tril. 49.35 za Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, ili iweze kutekeleza vipaumbele vyake vitano ilivyopanga kuvitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Ameeleza kuwa kati ya kiasi hicho kinachoombwa, sh. tril.29.42 zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Misaada na mikopo inatarajiwa kuwa sh.tril. 5.13, mikopo ya kibiashara kutoka nje na ndani ya nchi inakadiriwa kuwa sh. tril. 9.60 na maduhuli ni shi.bilioni 45.01.

“Kwa mwaka 2024/25, Wizara ya Fedha inaomba kuidhinishiwa matumizi ya sh. tril. 18.17 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mafungu nane (8) ya kibajeti. Kati ya kiasi hicho, shil. tril. 17.63 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha huduma ya deni la Serikali shil. tril. 13.13, mishahara sh. bilioni 946.45, matumizi mengineyo sh. bilioni 937.30 kwa mafungu ya Wizara na Taasisi zake, Huduma za Mfuko Mkuu sh. tril. 2.61 na matumizi ya maendeleo sh. bilioni 544.05” alisema Dkt.Nchemba.

Aliliomba Bunge kuidhinisha pia bajeti ya Fungu 045 linalohusisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iidhinishiwe jumla ya sh. bilioni 112.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya kiasi hicho, sh.bilioni 101.26 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. bilioni 11.47 matumizi ya maendeleo.

Alivitaja vipaumbele vitano vya mafungu ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/25 kuwa ni pamoja na kutafuta na kukusanya mapato ya sh. tril. 44.19 kati ya maoteo ya sh. tril. 49. 35 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali; Kuimarisha na kusimamia mifumo ya mapato, matumizi na mali za Serikali ikiwemo IDRAS, TANCIS, MUSE, NeST, CBMS na GAMIS; Kuhudumia deni la Serikali kwa wakati na kuboresha kanzidata ya kutunza taarifa za deni la Serikali,Kutoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za fedha nchini; na Kujenga uwezo kwa wakaguzi wa ndani, kamati za ukaguzi pamoja na waratibu wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn