logo

PROF.KABUDI AZINDUA KITUO CHA HUDUMA KWA MTEJA MoCLA JIJINI DODOMA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Wizara yake imejipanga kutatua kero za wananchi bila kuwalazimu kufika ofisi za Wizara kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja.

Prof. Kabudi ameyasema hayo alipokuwa kwenye hafla ya kuzindua kituo cha Huduma kwa Mteja leo tarehe 05 Septemba, 2024 katika Ofisi za Wizara Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambapo yeye alikuwa Mgeni Rasmi.

“Kupitia namba ya simu 026 216 0360 mwananchi anaweza kuwasilisha lalamiko lake na lalamiko hilo kufanyiwa kazi kwa wakati na kwa ufanisi bila mwananchi kulazimika kufika ofisi za Wizara. Huduma hii inasaidia kuwafikia wananchi wengi hususan wasio na uwezo wa kumudu gharama za usafiri kuja kuwasilisha malalamiko yao wizarani.” Alisema.

Amesema Wizara imeanzisha kituo hicho kupitia Programu ya Kujenga Uwezo wa Taasisi katika Kupambana na Rushwa (Building Sustainable Anti-Corruption Action in TanzaniaBSAAT) ili kupokea taarifa na malalamiko yanayohusu tuhuma za rushwa, ukiukwaji wa haki unaofanywa na taasisi ama mtu mmoja mmoja na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na Wizara pamoja na Taasisi zote zilizo katika mnyororo wa utoaji haki.

"Kituo hiki kimeanza kufanya kazi mwezi Februari, 2024 na hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2024 jumla ya malalamiko 499 yamesajiliwa, kati ya hayo malalamiko 410 sawa na asilimia 82 yamefanyiwa kazi kwa ukamilifu na 89 sawa na asilimia 18 yako katika hatua mbalimbali ya utekelezaji wake, Kwa sasa Kituo kinafanya kazi masaa yote ya kazi ila upo mpango wa kuongeza muda wa kutoa huduma kituoni hadi masaa 24 katika siku saba za wiki" alisema Prof.Kabudi.

.

Naye Mkurugenzi wa Idara Katiba na Ufuatiliaji Haki Bi. Jane Lyimo (aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Eliakim Maswi) amesema Kituo hicho kimeanzishwa baada ya Wizara kubaini kuwa malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakiwasilishwa wizarani kwa njia ya barua au wananchi hao kufika moja kwa moja kwenye ofisi za Wizara kwa kutumia gharama kubwa za usafiri na kujikimu.

.

Bi. Jane amesema uwepo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo inaendeshwa na Wizara katika maeneo mbalimbali nchini imeibua uwepo wa malalamiko na hoja mbalimbali za kisheria kwa wananchi ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn