TANZANIA NI NCHI YA KWANZA AFRIKA KUWEKA USTAWI WA WATOTO NJITI KATIKA MAZINGIRA SALAMA -DORIS MOLLEL
Mtandao wa Haki ya Afya ya Uzazi nchini (SRH) unaoongozwa na Doris Mollel Foundation kwa pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) wametoa pongezi kwa Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia na kupitisha sheria kuhusu nyongeza ya siku za likizo kwa wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti ambayo inaenda kusaidia kulinda ustawi wa watumishi wanaojifungua Watoto njiti nchini kwani jambo hilo lilikuwa ni changamoto kubwa na kilio cha muda mrefu cha Wafanyakazi Wanawake.
.
Makamu Mwenyekiti TUGHE, Dkt. Jane Madete akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 03,2025 Jijini Dar es Salaam, amesema hatua hiyo itasaidia kulinda ustawi wa watumishi wanaojifungua Watoto njiti nchini kwani jambo hilo lilikuwa ni changamoto kubwa na kilio cha muda mrefu cha Wafanyakazi Wanawake wanaopata changamoto ya kujifungua watoto njiti.
.
Amesema wafanyakazi wanawake wanaojifungua watoto njiti wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ikiwemo za kiafya hivyo wanahitaji kupata muda mwingi wa kupumzika na pia kumuhudumia mtoto toka katika kipindi cha uangalizi hadi wanaporuhusiwa kutoka hospitalini.
"Mbali na changamoto ya kiafya pia wamekuwa kwenye wasiwasi mkubwa wa kupoteza Ajira zao jambo ambalo linaweza kupelekea msongo wa mawazo na hata kuathiri kwa kiasi kikubwa malezi ya mtoto aliyezaliwa" alisema.
.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel amesema ni jambo jema kuona serikali inaendelea kuunga mkono juhudi za kusaidia mtoto njiti na Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika kupata mabadiliko haya katika sheria hii ambayo inaweka ustawi wa watoto njiti katika mazingira salama.
.
Amesema hadi kufikia mafanikio haya wamekuwa wakipambana kwa muda mrefu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo TUGHE hadi kufikia hivi sasa.
“Tunawashukuru TUGHE ambao walikuwa tayari kulipokea wazo na kulifanya kuwa la kwao, kwahiyo sasa likahama kutoka wazo la taasisi moja na kuhamia kwao, hii imetufunza kuwa kufanya kazi peke yako utafanikiwa kwa kuchelewa zaidi lakini mkiwa wengi inakuwa ni rahisi" alisema Doris.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

