logo

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATANGAZA ‎KUTOGOMBEA TENA UBUNGE JIMBONI RUANGWA

WAZIRI MKUU, na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Mhe. Kassim Majaliwa leo Julai 02,2025 ametangaza rasmi kutokugombea tena ubunge wa jimbo la Ruangwa baada ya kulitumikia jimbo hilo kwa miaka 15.

‎Akizungumza na wajumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao amekuwa mbunge wa jimbo hilo.

‎"Imefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili Kauli mbiu yetu ya Ruangwa kwa maendeleo inawezekana iweze kusonga mbele zaidi." alisema.

‎Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa wajumbe wa kamati ya siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote wenye nia ya kugombea ubunge wa jimbo hilo.

‎Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi Wana-Ruangwa kuendelea kushikamana na itakapofika siku ya uchaguzi waweze kuchagua wagombea wote watakaowakilisha chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi huo.

‎"Viongozi wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dkt. Nchimbi watakapokuja tujitokeze kwa wingi kwenye mikutano tusikilize sera, lakini siku ya kupiga kura tuwapigie kura nyingi za kutosha." alisema Majaliwa.

‎Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Viongozi wakuu wa chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwatumikia wana Ruangwa.

‎Mheshimiwa Majaliwa alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mwaka 2010 na amehudumu kwa kipindi cha miaka 15.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn