BMH,UDOM WAJENGEA UWEZO BUGANDO HUDUMA YA UPANDIKIZAJI FIGO
Jopo la wataalamu 12 likiwemo Madaktari Bingwa, wauguzi pamoja na wataalamu wa usingizi na ganzi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wamefanikisha zoezi la kuwajengea uwezo wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na kwa pamoja kufanikisha upandikizaji wa figo kwa mgonjwa wa kwanza katika hospitali hiyo.
.
Upasuaji huo wa kihistoria umefanyika kwa mwanaume mwenye umri wa miaka 40, mkazi wa Mkoa wa Mwanza, kwa ushirikiano wa karibu wa timu hizo tatu za kitaalamu.
.
Mkurugenzi Mkuu wa Bugando, Sr. Dkt. Alicia Massenga, ametoa shukrani kwa BMH na UDOM kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha hatua hiyo.
.
“Tunawashukuru sana wenzetu kutoka BMH kupitia Mkurugenzi Prof. Abel Makubi na Makamu Mkuu wa UDOM Prof. Lughano Kusiluka kwa kuruhusu timu hii kuja kutujengea uwezo. Huu ni uthibitisho kuwa ushirikiano baina ya hospitali hizi unaokoa maisha ya Watanzania,” amesema Sr. Dkt. Massenga.
.
Daktari Bingwa Mbobezi wa Figo kutoka BMH, Dkt. Sabina Mmbali, amesema programu hiyo ya ushirikiano ilianza miaka miwili iliyopita kwa lengo la kuiwezesha Bugando kuanza kutoa huduma ya upandikizaji figo hatua kwa hatua hadi kufikia mafanikio ya Aprili 16, 2026.
.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utaendelea hadi Bugando itakapokuwa na uwezo kamili wa kutoa huduma hizo kwa kujitegemea.
.
Kwa upande wake, Kiongozi wa jopo la wataalamu hao, Prof. Masumbuko Mwashambwa kutoka BMH na UDOM, amesema awamu ya kwanza ya programu hiyo ilikuwa ni tathmini ya kina ya uwezo wa Bugando ikihusisha miundombinu, vifaa tiba, dawa, vipimo na timu ya wataalamu.
.
“Baada ya kujiridhisha kuwa maandalizi yote yamekamilika, tulianza maandalizi ya wagonjwa na ndugu wachangiaji wa figo pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa timu ya Bugando. Hatimaye tukafanikisha kupandikiza figo kwa mgonjwa wa kwanza kwa mafanikio,” alisema Prof. Mwashambwa.
.
Hatua hii ni mafanikio makubwa ndani ya mkakati wa miaka kumi wa BMH wa kuzijengea uwezo hospitali nyingine nchini na kusogeza huduma za kibingwa karibu zaidi na wananchi.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

