logo

WAZIRI MKUU MAJALIWA ATOA MAAGIZO "IFIKAPO MWEZI OKTOBA MWAKA HUU UJENZI UWE UMEKAMILIKA"

WAZIRI Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameagiza kuwa ifikapo Oktoba mwaka huu, mradi wa majengo ya wizara mbalimbali unaoendelea katika mji wa Serikali uwe umekamilika na kuwekwa thamani, ili azma ya Serikali ya watumishi kuhamia kwenye majengo hayo ifikapo Januari Mosi, 2024 itimie.

Pia,Majaliwa amewataka wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa mradi huo wahakikishe wananunua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini lengo likiwa ni kuokoa fedha za kigeni pamoja na kuongeza tija katika uwekezaji.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Julai 03, 2023 baada ya kukagua ujenzi wa Mji wa Serikali na uwanja wa Mashujaa, Mtumba jijini Dodoma.

.

“Dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutaka kuona watumishi wote waliohamia Dodoma wanafanya kazi kwenye majengo rasmi.”

“Tafuteni mbinu za kiufundi za kukamilisha majengo haya kwa wakati bila kuathiri viwango ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi huu usiku na mchana, tunataka tumalize majengo haya, Watanzania wanataka kuona majengo yanakamilika na kutumika.” Amesema Majaliwa.

Wakati huo huo, Majaliwa amewataka wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo watumie bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini.

.

“Rais Dkt. Samia amesisitiza kuhusu uwekezaji na amekuwa akialika wawekezaji wa nje na wa ndani kujenga viwanda vya bidhaa mbalimbali hapa nchini ikiwemo marumaru (tiles). Tutumie bidhaa zao badala ya kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.”

@msemajimkuuwaserikali

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn