logo

DKT.BITEKO MGENI RASMI MAONESHO YA 6 YA MADINI MKOANI GEITA

NAIBU Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya Sita ya Madini mkoani Geita yatakayofunguliwa Septemba 23 mwaka huu katika Halmashauri ya Mji wa Geita huku Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kufunga maonyesho hayo Septemba 29 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya EPZA vilivyopo katika Kata ya Bombambili Halmashauri ya Mji wa Geita, Mkuu wa Mkoa huo Martin Shigela amesema,maonyesho ya mwaka huu yamekuwa na mwitikio mkubwa kutoka na washiriki wengi zaidi kujitokeza kuonyesha shughuli wanazozifanya katika sekta ya madini zikiwemo za uchimbaji,uchenjuaji na uongezaji thamani wa Madini hapa nchini.

“Maonyesho haya yalianza 2018 na mwaka huu ni maonyesho ya sita ya madini ambapo dhamira ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maarifa mapya watakayoyatumia katika shughuli za utafiti,kuongeza thamani na shughuli za uchenjuaji wa madini yetu hapa nchini,

“Kwa hiyo ukiangalia utaona mwaka huu mwitikio umekuwa mkubwa zaidi maana Mwaka jana tulikuwa na washiriki 250 ,lakini mwaka huu washiriki walioingia mpaka sasa ni zaidi ya 400 maana yake mwitikio ni mkubwa na wananchi hasa wachimbaji wameelewa maana ya uchimbaji hususan makampuni yanayojihusisha na uchimbaji,uchenjuaji ,uongezaji thamani kwa maana kwamba wameona umuhimu wa kushiriki katika maonyesho haya.”amesema Shigela.

Aidha, amesema Mkoa umeweka mazingira mazuri ili kuwawezesha wadau wa sekta ya madini kuja na teknlojia mpya na rahisi zitakazowawezesha wachimbaji wadogo kufaidika na teknolojia hizo kwa kuwa na gharama ndogo za uchimbaji,uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini ili nchi ifikie hatua ya kuhifadhi dhahabu ambayo imeongezwa thamani kwa zaidi ya asilimia 100.

Mkuu wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi hasa wanaojishughulisha na uchimbaji,uongezaji thamani na uchenjuaji wa madini kufika katika viwanja hivyo kujifunza na kujionesha mitambo na mshine kwa ajili ya shughuli za uchimbaji.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn