logo

WANAFUNZI 188,787 WALIOKIDHI VIGEZO WACHAGULIWA KUJIUNGA NA KUPANGIWA KIDATO CHA TANO PAMOJA NA VYUO VYA KATI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema jumla ya wanafunzi wote 188,787, waliokidhi vigezo wakiwemo wanafunzi wenye Mahitaji Maalum 812 wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na Kidato cha Tano katika shule mbalimbali nchini pamoja na vyuo vya kati katika fani mbalimbali.

.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Mei 30,2024 alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya uchaguzi wa Wanafunzi wa kujiunga na kidato cha Tano na vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa mwaka 2024 Jijini Dodoma.

.

Amesema kuwa muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza tarehe 1 Julai, 2024 hivyo, Wanafunzi wote waliopangwa kujiunga na Kidato cha Tano kwa mwaka, 2024 wanapaswa kuanza kuripoti Shuleni kuanzia tarehe 30 Juni, 2024 na Siku ya mwisho ya kuripoti itakuwa tarehe 14 Julai, 2024.

.

Waziri Mchengerwa amesema kwa wanafunzi waliopangwa kwenye Vyuo vya Elimu ya Ufundi watapokea maelekezo ya namna ya kujiunga kutoka katika Vyuo walivyopangwa na uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi umefanyika kwa kuzingatia ufaulu na nafasi zilizopo katika Shule; hivyo, hakutakuwa na fursa ya kufanya mabadiliko yoyote ya Shule kutokana na ukosefu wa nafasi.

.

Aidha,Mchengerwa ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa azma ya Serikali ya kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano katika kila Tarafa inatekelezwa, ili kuwezesha wanafunzi wote wanaofaulu Mtihani wa Kidato cha Nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Sita.

"Upanuzi na ujenzi wa Shule Mpya za Kidato cha Tano na Sita uendelee kufanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza tahasusi za masomo ya Sayansi. Mikoa ihakikishe inakuwa na tahasusi zote za msingi katika shule zake ili kuwapunguzia wazazi/walezi

za wanafunzi gharama za usafiri kwenda shule za mbalimbali" alisema Mchengerwa.

.

Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa na Fomu za kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Elimu ya Ufundi mwaka, 2024 inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi www.nactvet.go.tz.

#JordanMediaupdates

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn