DUWASA YATAKIWA KUKAMILISHA MRADI NDANI YA SIKU 21
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kuhakikisha kazi ya Uendelezaji wa Kisima cha Kisasa-Mwangaza pamoja na Usambazaji wa Huduma ya Majisafi kwa wananchi wa maeneo ya Kisasa, Mwangaza na Nyumba 300 inakamilika ndani ya wiki tatu.
Mhe. Shekimweri ametoa maagizo hayo Leo Oktoba 27, 2024 wakati wa Ziara ya Viongozi wa Wilaya ya Dodoma Mjini kukagua utekelezaji wa miradi ya maji, akiwemo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, Mwenyekiti wa CCM,Wilaya ya Dodoma Mjini, Charles Mamba na Diwani wa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega.
Mhe. Antony Mavunde ni Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Maji, ikiwemo miradi ya kimkakati katika Jiji la Dodoma ikizingatiwa ukuaji wa kasi wa Jiji kwa sasa.
Kadhalika, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Charles Mamba na Diwani wa Kata ya Nzuguni, Aloyce Luhega wameipongeza DUWASA kwa utekelezaji wa mradi wa Uchimbaji wa visima vya maji pembezoni mwa Jiji la Dodoma kwa kuwa maeneo hayo yana uhitaji mkubwa wa huduma ya maji.
DUWASA itatekeleza mradi wa uchimbaji wa visima 10 vya maji pembezoni mwa Jiji la Dodoma ambapo uchimbaji na uendelezaji wa kisima cha Kisasa-Mwangaza utagharimu shilingi Milioni 322.
Aidha, Uendelezaji wa kisima cha Kisasa-Mwangaza utaboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wapatao 28,000 wa maeneo ya Kisasa, Mwangaza na Nyumba 300 na unatarajiwa kukamilika kwa kipindi kisichozidi wiki nne kuanzia sasa.
Kisima cha Maji cha Kisasa-Mwangaza kina urefu wa mita 152 na kina uwezo wa kuzalisha maji lita 120,000 kwa saa, sawa na lita 2,880,000 kwa siku.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

