DORIS MOLLEL,GLOBAL FUND KUREJESHA SHULE WASICHANA WALIOKATISHA MASOMO
Taasisi ya Doris Mollel kwa kushirikiana na Global Fund inatarajia kuanza utekelezaji wa mradi maalum wa kusaidia wasichana wa rika balehe na wanawake vijana waliokatisha masomo kurejea katika mfumo rasmi wa elimu, hususan wale walioacha shule kutokana na ujauzito na changamoto nyingine za kijamii.
.
Mradi huo wa miezi sita utatekelezwa katika mikoa 15 na halmashauri 47 nchini, ukiwalenga pia wasichana wanaokimbia ukatili wa kijinsia kwa kuwapatia hifadhi katika nyumba salama.
.
Lengo ni kurejesha matumaini ya elimu, kulinda utu wa mtoto wa kike, na kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha kundi hilo kuendelea na masomo bila vikwazo.
Aidha, kupitia utekelezaji wa mradi huo, taasisi hiyo inalenga kuzishawishi baadhi ya halmashauri kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa taulo za kike shuleni ili kupunguza changamoto zinazowakwamisha wasichana kuhudhuria masomo wakati wa hedhi.
.
Akifungua kikao kazi cha wadau na maofisa wa Serikali kilichofanyika Aprili 28, 2026, Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Afya Tanzania, Bw. Paul John, amesema wizara inatambua mchango mkubwa wa wadau katika kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI na kulinda afya za wasichana rika balehe, kundi ambalo bado linaathirika zaidi.
.
Amesema bila mikakati madhubuti ya ulinzi kwa wasichana, Taifa litaendelea kupoteza nguvu kazi ya baadaye kutokana na ongezeko la maambukizi katika kundi hilo.
.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Doris Mollel, amesema kupitia majukwaa ya wadau zaidi ya 100 yanayofanyika kila mwaka, wamekuwa wakijadili changamoto zinazowakabili vijana, ikiwemo upatikanaji wa huduma rafiki, bidhaa za hedhi kwa gharama nafuu, na fursa za kurejea shule kwa wasichana waliopata ujauzito.
.
Amesema mradi huo ni wa matumaini kwa mtoto wa kike kwani unalenga si tu kurejesha elimu yake bali pia kulinda utu na hadhi yake kupitia huduma za nyumba salama na mazingira bora ya kujifunzia.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

