KAMATI YA USTAWI ZANZIBAR YAJIFUNZA UTENDAJI WA NACTVET JIJINI DODOMA
Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imetembelea Makao Makuu ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) jijini Dodoma tarehe 29 Aprili 2026, kwa lengo la kujifunza namna taasisi hiyo inavyosimamia ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Ujumbe huo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Dkt. Nasra Nassor Omar, ambaye alisema ziara hiyo itaiwezesha Kamati kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa elimu ya ufundi na kusaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khadija Salum Ali, alieleza kuwa ziara hiyo itapanua wigo wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu za Zanzibar na Bara, hasa katika kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu ya ufundi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Ibrahim Lingwanda, aliushukuru ujumbe huo na kusisitiza dhamira ya NACTVET kuendeleza ushirikiano na kuyafanyia kazi masuala yote yaliyojadiliwa ili kuimarisha sekta ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Ziara hiyo pia ilihusisha viongozi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania Bara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi katika sekta ya elimu.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news

