logo

DKT.NCHIMBI: KATENDENI HAKI KUPATA VIONGOZI WALIO BORA NA WANAOCHAGULIKA

Na Deborah Lemmubi-Dodoma.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi ametaka Chama kufanya jitihada za kupata wagombea wenye sifa za kutimiza majukumu yao,wanaochagulika na pia wanaokubalika katika jamii na wasio na makando makando katika jamii zao ili waweze kuaminiwa kuongoza katika Nchi yetu,kwani ushindi wa Chama hicho unategemea na aina ya wagombea wanaopatikana.

Dkt. Nchimbi ameyasema hayo jana Februari 19,2025 Jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya Watendaji wa Kata na Makatibu Tawi wa Mkoa wa Dodoma.

Sambamba na kutuma salamu kwa wale wote walioanza vikao na kutoa matamko ya kutaka kupita bila kupingwa katika Chaguzi kwani kitu hicho hakipo na utaratibu uliopo ni kila mtu kugombea.

"Ushindi wa Chama chetu unategemea na aina ya wagombea wanaopatikana,lazima Chama kifanye jitihada ya kupata wagombea wenye sifa na kuweza kutimiza majukumu yao,vile vile wanaochagulika,wanaokubalika na jamii wasio na makando makando katika jamii zao ambao jamii inaweza kuwaamini kwamba hawa wanaweza kuongoza katika nchi yetu.

"Na ndio maana basi katika Mkutano Mkuu wa CCM uliopita tulifanya mabadiliko makubwa ya mfumo ya kupata wagombea wetu na kuongeza idadi ya wapiga kura ambayo itapelekea kupunguza mianya ya rushwa". alisema.

Sambamba na hayo Dkt. Nchimbi amewasihi wana CCM kuhakikisha wanatumia mwaka huu wa uchaguzi 2025 kupata viongozi safi na bora wanaochagulika, na kusimamia na kutenda haki kwa Nchi kwani kwa kufanya hivyo Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuwa imara na kuaminiwa na wananchi na kuendelea kushika dola Tanzania.

"Nilitamani kutumia nafasi hii kuwasihi wana CCM kufanya kila inavyowezekana kuhakikisha tunatumia mwaka huu kupata viongozi safi na bora,kupata viongozi wanaochagulika nchi nzima kwa kusimamia kanuni, Katiba pia tendeni haki, Mkiweza kusimamia haki basi Chama chetu kitaendelea kuwa imara na kuaminiwa na wananchi na kuendelea kushika dola Tanzania na kudumisha amani na upendo kwa muda mrefu". Alisema.

Aidha,amewataka Viongozi kufanya kazi kwa bidii ili katika chaguzi waweze kupimwa kwa kazi na maendeleo waliyoyaleta na sio kwa kiwango cha kutoa rushwa, kwani kwa mabaliko yaliyofanywa ndani ya Chama cha Mapinduzi rushwa imepata majeraha ya kudumu.

"Ukichaguliwa kafanye kazi ili baada ya miaka mitano upimwe kwa kazi uliyofanya,upimwe kwa maendeleo uliyoleta,hatuwezi kukupima kwa viwango vya kutoa rushwa ,kwamba wewe ndio kiongozi bora kwasababu tunajua unatugawia kiasi fulani cha fedha. Tunaamini kwa mabadiliko tuliyoyafanya ndani ya CCM na wagombea wa CCM rushwa imepata majeraha ya kudumu,lakini watu wote ambao ni wachapa kazi wamefurahishwa na mabadiliko hayo ambayo hayawapi nafasi wagawa pesa".

Kwa upande Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini Bwana Charles Mamba amesema kuwa neno haki lina herufi nne tu lakini lina maana kubwa hivyo kama alivyoagiza Katibu Mkuu wakatende haki ili wale viongozi wenye sifa ya kuwa viongozi lakini hawana kipato au fedha ya kutoa rushwa wakapate nafasi ya kuongoza kupitia haki.

Lengo la Mafunzo haya ni kujenga uelewa kwa Viongozi ngazi mbalimbali wa Kata na Makatibu tawi ndani ya Chama cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi Mkuu hapo baadae 2025.

Frank Jordan
12345 123
Follow Us
logo

© 2023 Jordan Media. All Rights Reserved. Designed by Lylical Popcorn