
KASA: VIUMBE WALIOPO HATARINI KUPOTEA KUTOKANA NA BINADAMU KUWAFANYA KITOWEO
Kila ifikapo tarehe 17 mwezi Juni kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya Kasa lengo kuu likiwa ni kuwalinda na kuwatunza kutokana na viumbe hao kuliwa na binadamu licha ya kuwa na umuhimu mkubwa kwa viumbe wengine wa baharini.
.
Kutangazwa kwa siku hiyo kunatokana na umuhimu wa viumbe hao baharini ambapo pia wamekuwa wakipungua kutokana na kuliwa na binadamu ili hali wana sumu katika miili yao inayotokana na vyakula wanavyokula.
Kasa ni moja kati ya mamilioni ya viumbe wa ajabu wanaoishi baharini ambapo kwa upande mwingine unaweza kusema ni Kobe anayeishi majini.
.
Mwongozaji watalii kutoka Unguja visiwani Zanzibar ambaye pia ni mfanyakazi wa Nungwi Mnarani Aquarium Bw.Isaack Samwel, amesema Kasa ni kiumbe ambaye anaishi miaka 120, na anabalehe akifikisha umri wa miaka 25 huku utagaji wa mayai kwa viumbe hao ni mara moja tu kwa mwaka, na mara sita/saba kipindi chote cha uhai wao.
.
"Kasa anataga mayai 100-200, na joto la mchanga pekee linatumika kuangua (kutotoa) watoto, na pia joto la mchanga hutumika kutambua ya kwamba kasa ni jike au dume.
.
"Joto linapokuwa juu zaidi kwenye kiota wengi huzaliwa jike, na linapokuwa chini kidogo huzaliwa dume" alisema.
.
Kwa upande mwingine, Bw.Isaack amesema Kasa ni kiumbe ambaye yupo kwa ajili ya kupendezesha bahari na kupendezesha vitu vya asili vilivyopo ndani ya bahari hivyo huwa haliwi kama chakula.
.
"Kasa ni samaki ambaye haliwi, na ni Kutokana na vyakula anavyokula ambavyo huwatengenezea sumu mwilini mwao.
.
"Sasa unapokuwa haujui tofauti ya aina ya kasa,hii hupelekea kula kasa mwenye sumu na kukuleta madhara" alisema Isaack.
.
Bwawa la Mnarani Aquarium lililopo eneo la Nungwi, Zanzibar lilianzishwa mnamo mwaka 1993, na mvuvi aliyefahamika kwa jina la Baba Kasa "Mzee Mataka" ambaye alianzisha mradi wa kutunza Kasa mara baada ya kuona jamii ya viumbe hao wameanza kupotea kutokana na wavuvi wenzake wanapokuwa wanamkamata na kumfanya kitoweo.
Tranding News
Newsletter
Subscribe to our newsletter to get the latest news